Umoja wa Mataifa na wenza wake wa kibinadamu waonya kuhusu ongezeko la wakimbizi wa ndani nchini DRC
2024-05-01 08:45:29| CRI

Umoja wa Mataifa na wenza wake wa kibinadamu umeonya kuwa ongezeko la mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) linasababisha ongezeko la idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.

Katika taarifa iliyotolewa jana na viongozi wa mashirika 20 ya kibinadamu wakiongozwa na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Kibinadamu, Martin Griffiths, viongozi hao wamesema, katika miezi michache iliyopita, zaidi ya watu 700,000 wamelazimika kukimbia makazi yao, na kufanya idadi ya watu waliokimbia makazi yao kufikia milioni 7.2, kiasi cha juu zaidi kuwahi kutokea.

Taarifa hiyo imesema, uhalifu wa kijinsia umefikia kiwango cha juu zaidi, huku rekodi ikiongezeka kati ya mwaka 2022 na 2023, na kwamba hofu ya kisasi na kunyanyapaliwa kunawafanya waathirika wengi kushindwa kutoa taarifa.

Aidha, licha ya uhalifu wa kingono, watoto pia wako hatarini kutokana na matishio mengine ikiwemo kutekwa nyara, kuuawa, kuteswa na kuandikishwa kama wapiganaji na makundi yenye silaha.