Msemaji wa serikali ya Kenya Isaac Mwaura amesema, watu 179 wamefariki, wakiwemo watu wazima 164 na watoto 15, kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana jijini Nairobi, Mwaura amesema, watu wengine 90 hawajulikani walipo, na zaidi ya watu 124 wamejeruhiwa na wanapata matibabu katika hospitali mbalimbali nchini humo. Amesema mvua hizo na mafuriko zimesababisha watu 188,000 kukosa makazi, na kuilazimu serikali kuanzisha kambi za muda ili kutoa makazi kwa watu hao.
Jumanne wiki hii, Baraza la Mawaziri la Kenya liliwaamuru wakazi wa maeneo yaliyo hatarini kukumbwa na mafuriko nchini humo kuondoka kwa hiari ama kuondolewa kwa lazima. Maeneo hayo ni pamoja na yale yaliyopo karibu na mabwawa na hifadhi nyingine za maji katika ardhi za umma ama binafsi, maeneo yaliyo hatarini kukumbwa na maporomoko ya udongo, na maeneo ya kando ya mito na njia nyingine za maji nchini humo.