China yasema njama ya Marekani kuidhibiti China kwa kutumia suala la Taiwan haitafanikiwa
2024-05-03 09:16:27| CRI

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesisitiza kuwa kanuni ya China Moja ni kanuni inayokubalika na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, haipingiki na wala haizuiliki, na njama yoyote ya kuidhibiti China kwa kutumia suala la Taiwan hakika itapingwa kithabiti na jumuiya ya kimataifa, na haitafanikiwa.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bw. Antony Blinken kutoa taarifa Mei Mosi kuwa Marekani inaliunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO) kuialika Taiwan kuhudhuria mkutano wa mwaka huu wa Baraza la Afya Duniani (WHA) kama mwangalizi.

Wizara hiyo imesema, suala la Taiwan likiwa sehemu muhimu ya maslahi ya China, ni mstari mwekundu wa kwanza usiovukika wa uhusiano kati ya China na Marekani, na kuitaka Marekani itekeleze kivitendo ahadi iliyotolewa na viongozi wa nchi hiyo ya kutounga mkono “Taiwan kujitenga na China”.