Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ikionya kuwa maendeleo ya binadamu katika Ukanda wa Gaza yatarudi nyuma kwa miaka 44 kama vita ya hivi sasa itaendelea kwa miezi 9.
Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Kamati ya Uchumi na Jamii kanda ya Asia Magharibi (ESCWA) zimekadiria kuwa katika miezi saba ya vita, Fahirisi ya Maendeleo ya Binadamu (HDI) katika Ukanda wa Gaza itapungua hadi kufikia 0.582, ikirudisha nyuma maendeleo kwa miaka 37.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kama vita itadumu miezi tisa, maendeleo ya binadamu ya miaka 44 yatafutwa kabisa, yakirudisha nyuma hali ya Ukanda wa Gaza katika viwango vya mwaka 1980.
Wakati vita ikiingia katika mwezi wa saba, kiwango cha umaskini cha Palestina kitafikia asilimia 58.4, ambapo watu wengine milioni 1.74 wataangukia katika umaskini.