UM waeleza wasiwasi wake kutokana na vurugu katika mkoa wa Darfur Kaskazini nchini Sudan
2024-05-03 08:31:25| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya kibinadamu (OCHA) imesema, ina wasiwasi na mapigano na kuongezeka kwa mvutano unaotishia raia ndani na karibu na El Fasher, mji mkuu wa mkoa wa Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Ofisi hiyo imesema imeshtushwa kuhusu vizuizi kwa mienendo ya raia na ripoti za raia kushambuliwa na kuporwa wakati wakijaribu kukimbilia sehemu ya kusini ya mji huo.

Ofisi hiyo imeonya kuwa, mapigano makali katika mji wa El Fasher yatawaweka hatarini raia zaidi ya 800,000, wakiwemo wakimbizi wa ndani zaidi ya laki 2 tangu kuanza kwa vita nchini Sudan mwaka mmoja uliopita.

Pia OCHA imesema, mapigano ndani na maeneo ya pembezoni ya mji huo yamesababisha kusitishwa kwa njia za kupeleka misaada kwa raia wanaohitaji msaada, na kuongeza kuwa kama vurugu zikiendelea katika mji huo, zaidi ya watu 360,000 watakosa msaada wa chakula na mahitaji mengine ya maisha, na zaidi ya watu 100,000 watakosa hifadhi.