Kenya kuongeza hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi
2024-05-03 08:30:52| CRI

Baraza la Mawaziri nchini Kenya jana limeamua kuhamasisha wananchi wake kutekeleza sera, miradi na hatua zitakazosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baraza hilo lililokutana mara mbili ndani ya wiki moja chini ya uongozi wa rais wa Kenya William Ruto, limekubali kuwa mabadiliko ya tabianchi ni chanzo cha mafuriko na maporomoko ya udongo na hali nyingine mbaya za hewa.

Mkutano huo ulijadili hatua za kukabiliana na athari mbaya za mafuriko, maporomoko ya matope na maporomoko ya udongo, ambazo zimesababisha vifo vya watu 188 nchini humo.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Kenya pia zimesababisha uharibifu mkubwa wa madaraja, barabara, na miundombinu mingine muhimu nchini humo. Baadhi ya shule zimefungwa huku nyingine zikitumika kama kambi za muda kuwahifadhi watu waliopoteza makazi yao kutokana na mafuriko, maporomoko ya matope na maporomoko ya udongo.