Malawi yaanza kuuza soya nchini China
2024-05-06 08:40:18| CRI

Mazao ya soya ya Malawi  yamefanikiwa kuingia katika soko la China wakati nchi hiyo ikijaribu kuongeza mauzo ya nje ya mazao ya kilimo ili kukuza uchumi wake.

Akithibitisha kwa vyombo vya habari vya ndani siku ya Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji na Biashara cha Malawi Bw. Paul Kwengwere alisema shehena ya majaribio ya tani 240 za soya kutoka kampuni ya Paramount ilisafirishwa kwa mafanikio na kuidhinishwa na mamlaka husika ya China.

Aidha alisema haya ni mafanikio yaliyotokana na juhudi za wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashirika ya serikali, makampuni binafsi, na wawakilishi wa China.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Paramount Bw. Mahesh Ghedhia alisema, baada ya kupewa kibali cha uthibitisho wa ubora na mamlaka ya China, kampuni yake imesaini mkataba wa kuuza tani 20,000 za soya katika soko la China linalotafuta tani 100,000, na kwamba wana mpango wa kuongeza zaidi mauzo hayo.