Mvua yasababisha watu 400 kukosa makazi nchini Tanzania
2024-05-06 23:35:50| cri

Mvua kubwa iliyonyesha mfululizo kwa zaidi ya saa 72 katika mji wa Ifakara, wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro nchini Tanzania, imesababisha mafuriko makubwa na watu zaidi ya 400 kukosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji na nyingine kubomoka.

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyobya amesema mafuriko hayo yametokana na kujaa kwa Mto Lumemo na kumwaga maji yake katika makazi ya watu wanaoishi karibu na mto huo na sehemu ya katikati ya mji.

Amesema serikali ya huko imewaokoa wananchi ambao nyumba zao zimejaa maji na kuwatafutia sehemu salama ya kuishi kwa muda, ambapo watapewa msaada wa chakula na mahitaji mengine ya muhimu.