Rwanda yapinga tuhuma za Marekani kuhusu kuhusika kwake na shambulio katika kambi ya wakimbizi nchini DRC
2024-05-07 23:04:48| cri

Rwanda imepinga tuhuma za Marekani kuwa inahusika na shambulio la mabomu katika kambi ya wakimbizi wa ndani iliyoko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo watu 14 waliuawa.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makalo amesema katika taarifa yake kuwa, jaribio la Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuilaumu Rwanda moja kwa moja bila ya kufanya uchunguzi wowote kuhusu shambulio hilo haukubaliki, na kuongeza kuwa, Rwanda haitabeba wajibu wa shambulio hilo.

Watu 14 waliuawa na wengine 35 kujeruhiwa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, baada ya shambulio la mabomu katika kambi tatu za wakimbizi wa ndani zilizoko Lac Vert, Lushagala na Mugunga, pembezoni mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, nchini DRC, ijumaa iliyopita.