Kenya na Somalia zasaini makubaliano ya ushirikiano katika mashauriano ya kisiasa, elimu na ulinzi
2024-05-07 08:37:48| CRI

Kenya na Somalia Jumatatu zilisaini makubaliano ya ushirikiano katika nyanja za mashauriano ya kisiasa, elimu na ulinzi.

Akiongea kwenye kikao cha tatu cha tume ya pamoja ya Kenya na Somalia (JCC), Waziri Mkuu wa Kenya Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa mambo ya Nje na masuala ya Diaspora, alisema huko Nairobi, Kenya, kwamba nyanja hizo tatu zinalenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa nchi hizo mbili kwa manufaa ya watu wa nchi hizo mbili. Mudavadi aliongeza kuwa Kenya ina uhusiano wa kipekee na Somalia, sio tu kwa sababu wana mpaka mmoja bali pia kwa sababu ya ushirikiano wao imara na wa kudumu.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Somalia, Ahmed Moalin Fiqi, alisema kuwa nchi zote mbili pia zimefanya jitihada za kuimarisha ushirikiano katika nyanja za usalama, kujenga uwezo katika eneo la afya kwa kuongeza ujuzi wa wataalamu wa afya, pamoja na kuwapatia mafunzo maafisa wa polisi.