Rais wa Tanzania aagiza huduma za dharura kupelekwa kwenye maeneo yaliyokumbwa na kimbunga
2024-05-07 08:37:06| CRI

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameziagiza mamlaka kuchukua hatua za dharura ikiwa ni pamoja na kutuma vifaa vya msaada kwa wahanga katika maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya. 

Hayo yamesemwa Mei 6 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao cha dharura cha Kamati ya Maafa Kitaifa alichokiitisha ili kupokea taarifa za hatua zilizochukuliwa juu ya uharibifu uliosababishwa na kimbunga Hidaya katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani, wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na Ifakara mkoani Morogoro.

Jumapili, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Joseph Mwasabeja alisema mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana kutokana na kimbunga cha Hidaya kilichopungua baada ya kutua katika Kisiwa cha Mafia mapema Jumamosi, yalisomba madaraja manne.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mohamed Nyundo, alisema mafuriko hayo pia yamesababisha nyumba kadhaa katika vijiji saba kuzama na kusababisha wananchi wengi kupoteza makazi yao na kuharibu mamia ya hekta za mazao ya shambani.