Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres jana Jumanne alitoa wito tena kwa Israel na kundi la Hamas kuonesha “ujasiri wa kisiasa” na kufanya juhudi za kusitisha mapigano wakati mvutano katika Ukanda wa Gaza ukiendelea kuongezeka.
Bw. Guterres amesema hali katika Ukanda huo imezorota, haswa katika eneo la Rafah, ambako wakimbizi wa Palestina wamejaa. Pia amesema kufungwa kwa vivuko vya Rafah na Karem Shalom kumezorotesha hali ya kibinadamu ya Ukanda huo, akitaka vivuko hivyo vifunguliwe mara moja. Pia ameonya kuhusu matokeo mabaya kutokana na mapigano yanayoendelea na kusisitiza haja kwa pande mbili za mgogoro kuwasiliana kidiplomasia, badala ya kuzidisha mvutano.