Marais wa China na Ufaransa wafanya mazungumzo mkoani Hautes-Pyrénées
2024-05-08 09:16:12| CRI

Kutokana na mwaliko maalum wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Rais Xi Jinping jana Mei 7 aliondoka Paris na kuelekea mkoa wa Hautes-Pyrénées, kusini magharibi mwa Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo na Rais Macron.

Kwenye mazungumzo yao, Rais Xi amesema, China na Ufaransa zinaweza kushirikiana licha ya kuwepo tofauti kwenye ustaarabu, itikadi na mfumo wa kijamii, na kutoa mchango mpya kwa ajili ya amani na maendeleo ya dunia kwa kupitia mazungumzo na ushirikiano. Amesema China inapenda kuimarisha mawasiliano ya kiutamaduni na Ufaransa na Ulaya, kuendelea kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, kuzidisha maelewano na kuimarisha urafiki kati ya watu wa pande hizo mbili.

Rais Macron amesema, katika wakati huu ambapo hali ya kimataifa imejaa sintofahamu, ni muhimu kwa Ulaya kudumisha umoja na mshikamano na  kujiamulia kimkakati, na pia ni muhimu kwa Ulaya kukuza uhusiano na ushirikiano na China. Amesema Ufaransa na China zikiwa wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, anatarajia kudumisha mawasiliano ya karibu na Rais Xi, na kutoa mchango wa kuongeza hamasa katika kulinda amani na utulivu wa Ulaya na dunia.