FIilamu mpya ya kuitangaza Tanzania iitwayo ‘Amazing Tanzania’ inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi huu jijini Beijing, China ikiwashirikisha marais Samia Suluhu Hassan na Dk Hussein Mwinyi wa Zanzibar.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya Kutangaza Tanzania, Dk Hassan Abbasi alipokuwa katika moja ya maeneo iliporekodiwa filamu hiyo.
Alisema filamu hiyo itakuwa na maudhui mapya badala ya kuwa na mtangazaji kama ilivyokuwa katika ‘Royal Tour’ ambapo itakuwa na msanii Jin Dong ambaye atapitishwa na Rais Samia katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini Tanzania. Kuhusu sababu za uzinduzi kufanyika China, alisema ni nchi yenye idadi kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.5, lakini pia Wachina zaidi ya milioni 200 kwa mwaka hutoka kwenda sehemu mbalimbali duniani.
Alisema baada ya uzinduzi wa filamu hiyo Beijing, itaoneshwa katika miji ya Shanghai na Guangzhou na baadaye maeneo mengine yatatangazwa. Filamu hiyo ya kuitangaza Tanzania ni ya pili ikitanguliwa na Tanzania: The Royal Tour ambayo mhusika wake mkuu ni Rais Samia aliyeizindua jijini New York, Marekani.