Shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa zilitatizika Jumanne Mei 7, 2024 alasiri baada ya ndege iliyokuwa ikielekea Frankfurt, Ujerumani, kulazimika kutua kwa dharura.
Vyanzo vya habari vilivyoomba kutotajwa jina kwa kukosa mamlaka ya kuzungumzia tukio hilo vilisema ndege hiyo iliyokuwa na watu 266 ilipata hitilafu baada ya kugongwa na ndege wakati wa kupaa. Meneja wa uwanja wa ndege Abel Gogo alithibitisha tukio hilo siku ya Jumatano na kusema kuwa ndege hiyo bado inaendelea kutengenezwa.
Tukio hilo lililotokea saa 6.22 mchana, dakika mbili tu baada ya kupaa, liliathiri injini ya kushoto ya ndege hiyo. Timu za kudhibiti majanga ziliitikia haraka tahadhari hiyo na kutuma magari manane ya zima moto na zaidi ya magari 10 ya wagonjwa.