WanaTikTok wakamatwa kwa video ya mzaha kwenye kituo cha polisi huko Kilifi
2024-05-09 21:54:36| cri

Jaribio la kueneza mtandaoni TikTok lililofanywa na kundi la vijana wa Kilifi waliorekodi wizi kwa njia ya mzaha nje ya kituo cha polisi limeambulia patupu na badala yake kuwaingiza matatani. Hii ni baada ya kukamatwa Jumatano kwa madai ya kuchafua sifa ya Huduma ya Polisi ya Kenya.

Wanne hao, miongoni mwao akiwemo kijana mwenye umri wa miaka 17, walipiga na kuchapisha video kuhusu "wizi" uliokuwa ukifanyika nje ya kituo cha polisi katika Mji wa Kilifi. Bila kujua, maafisa wa polisi walikuwa wametazama video yao, iliyopewa jina la ‘wezi mbele ya kituo cha polisi’, kwenye TikTok.

Katika video hiyo, mwanamume anayeonekana kuwa mlevi anaibuka kutoka kwenye kantini ya Kituo cha Polisi na kuibiwa begi lake na watu wengine wawili kwenye boda boda.

Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao, Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Kilifi Kaskazini Kenneth Maina alisema video iliyosambaa ya wizi wa mchana katika kituo cha polisi cha Utawala wa Kilifi si ya kweli...ni mzaha wa kundi la vijana wanaotengeneza maudhui,”

WanaTikTok hao walikamatwa wakiwa nyumbani kwao Kilifi, huku mkubwa akiwa na umri wa miaka 27.

Polisi wanasema wanamsaka mshukiwa mwingine ambaye bado hajakamatwa.