Kenya yatoa wito wa kuwepo kwa amani endelevu nchini Sudan Kusini wakati mazungumzo yakiwa yameanza
2024-05-10 08:44:28| CRI

Rais wa Kenya William Ruto alifungua mazungumzo ya upatanishi siku ya Alhamisi kati ya pande zinazohusika katika mchakato wa amani wa Sudan Kusini, akitaka pande hizo kujizatiti ili kufikia amani endelevu.

Mazungumzo hayo yaliyopewa jina la Mpango wa Tumaini, yaliongozwa na Kamanda wa zamani wa Jeshi la Kenya, Lazurus Sumbeiywo, ambaye pia alikuwa mpatanishi wa Makubaliano ya Amani ya Kina (CPA) mwaka 2005 ambayo yalifungua njia ya uhuru wa Sudan Kusini.

Akifungua mazungumzo hayo mjini Nairobi Ruto alisema mchakato wa upatanishi una nia ya kumaliza mzozo na ukosefu wa utulivu wa kisiasa nchini Sudan Kusini kwani unajumuisha watu wote na ni wa nyumbani. Alisifu maendeleo yaliyofikiwa na Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa, Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan (SPLM), na Sudan Kusini United Front katika mchakato wa upatanishi.

Kwa upande wake rais wa Sudan Kusini Salva Kiir alisema serikali yake itashiriki katika mazungumzo hayo kwa nia njema na kwa moyo wazi, akitumai kuwa makundi ya upinzani yana nia kama hiyo na hamu ya amani nchini Sudan Kusini, ambayo ikipatikana kikamilifu, italeta utulivu wa milele na maendeleo ya kiuchumi katika kanda, na sio Sudan Kusini pekee.