Misri Jumapili ilitangaza kwamba "itaunga mkono rasmi" kesi ya mauaji ya halaiki iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu uvamizi unaoendelea wa Israel katika Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Tangazo hilo lililotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri, limekuja kutokana na "kuendelea kwa Israel kufanya mashambulizi dhidi ya watu wa Palestina, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia, kufanya uharibifu wa miundombinu katika eneo hilo, na kuwalazimisha Wapalestina kuhama kwenye ardhi yao."
Mashambulizi ya Israel "yamesababisha mzozo wa kibinadamu ambao haujawahi kushuhudiwa na kusababisha watu wasiweze kuishi katika Ukanda wa Gaza, kutokana na ukiukaji wa wazi wa vifungu vya sheria za kimataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Hata hivyo taarifa hiyo haikufafanua ni aina gani ya uungwaji mkono utakaotolewa kwa Afrika Kusini katika kesi hiyo. Ilikuja baada ya Afrika Kusini Ijumaa kuitaka mahakama ya ICJ kutoa amri mpya kwa Israel kusitisha mara moja operesheni yake katika Rafa na kujiondoa katika mji huu wa kusini mwa Gaza.