Israel yaamuru tena kuhamishwa kwa watu huko Rafah baada ya kura za UM kuunga mkono uanachama wa Palestina
2024-05-13 09:22:24| CRI

Israel Jumamosi ilitoa amri nyingine ya kuhamishwa watu katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah wakati ikijiandaa kuzidisha operesheni yake ya kijeshi, siku moja baada ya Umoja wa Mataifa (UM) kupitisha azimio la kuidhinisha ombi la Wapalestina la kutaka uanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.

Azimio hilo lililopitishwa kwa kura 143 za ndio na tisa zikipiga ya hapana, zikiwemo Marekani na Israel, huku nchi 25 zikijizuia, lilionesha uungaji mkono unaoongezeka kwa Wapalestina, huku nchi nyingi zikielezea kukerwa na kuongezeka kwa idadi ya vifo huko Gaza na kuwa na wasiwasi juu ya uwezekano mkubwa wa mashambulizi ya Israeli huko Rafah.

Zaidi ya Wapalestina milioni 1 waliokimbia makazi yao wanatafuta hifadhi Rafah, ambako janga kubwa la kibinadamu linakaribia kutokana na uhaba wa vitu muhimu kama vile maji, chakula na huduma za matibabu. Sasa, mji huo uko ukingoni kuwa na mgogoro mpya.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa uvamizi wa Rafah utazidisha mzozo wa kibinadamu na kusababisha kuongezeka kwa vifo vya raia.