Raia wasiopungua 27 wauawa katika mapambano mapya huko Darfur Kaskazini nchini Sudan
2024-05-13 09:18:40| CRI

Umoja wa Mataifa Jumapili ulisema raia wasiopungua 27 wameuawa na wengine takriban 130 kujeruhiwa kwenye mapambano yaliyotokea tena kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraha (RSF) huko El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Ripoti mpya iliyotolewa na Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) ilisema, ripoti zisizothibitishwa zimeonyesha kuwa watu wasiopungua 27 wameuawa wakiwemo wanawake na watoto, huku watu takriban 130 wakijeruhiwa. Hivi sasa hospitali ya El Fasher Kusini yenye vitanda 100 imeelemewa wagonjwa.

Ikinukuu ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kufuatilia Uhamiaji wa Wakimbizi, OCHA ilisema watu 850 (familia 170) wanakadiriwa kukimbilia sehemu mbalimbali huko El Fasher kutokana na mapambano hayo.