Nchi za Afrika zahimizwa kuboresha muunganisho wa anga ili kukuza utalii
2024-05-14 09:16:58| CRI

Waziri wa Utalii wa Afrika Kusini Patricia de Lille amesema nchi za Afrika zinapaswa kufanya kazi pamoja ili kuboresha muunganisho wa anga, ambao utakuza utalii na ukuaji wa uchumi.

De Lille aliyasema hayo Jumatatu jioni wakati wa Mazungumzo ya Mawaziri wa Utalii wa Afrika yaliyofanyika Durban nchini Afrika Kusini. Alisema Kampuni ya Viwanja vya Ndege ya Afrika Kusini (ACSA) itatumia randi bilioni 21.7 (kama dola bilioni 1.18 za Kimarekani) kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini Afrika Kusini.

Aliongeza kuwa dunia nzima iko tayari kufanya usafiri upatikane kwa urahisi zaidi, na vyanzo muhimu vya masoko kama vile China na India vinatarajiwa kuongezeka, hivyo amesisitiza ni lazima washirikiane ili kurahisisha kusafiri kwenda Afrika na ndani ya Afrika. Aidha amebainisha kuwa sasa ni wakati wa kufikiria upya mikakati ya maendeleo katika sekta ya utalii na kuimarisha mafungamano na ushirikiano wa kikanda.

Aliwataka mawaziri wa utalii wa Afrika kutafuta ufumbuzi madhubuti ili kutoa fursa za kuongeza muunganisho wa anga barani Afrika.