Kenya yasema juhudi zinaendelea kurejesha intaneti katika Afrika Mashariki kufuatia hitilafu katika waya wa chini ya bahari
2024-05-14 09:15:55| CRI

Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya (CA) ilisema Jumatatu kuwa juhudi za kurejesha huduma za mtandao wa intaneti ambazo zimekatika kote Afrika Mashariki zinaendelea.

Mamlaka hiyo ilithibitisha kuwa waya huo wa chini ya bahari ulikatika Jumapili katika kituo kinachounganisha mawasiliano ya simu cha Mtunzini nchini Afrika Kusini, na kuathiri nyaya kadhaa zinazohudumia Kenya, ukiwemo Mfumo wa Nyaya za chini ya bahari wa Afrika Mashariki (EASSy).

Katika taarifa iliyotolewa Nairobi, Kenya, Mkurugenzi Mkuu wa CA David Mugonyi alisema kwamba licha ya juhudi za kurejesha huduma hiyo, lakini usumbufu na kasi ndogo ya intaneti huenda ukaendelea katika siku chache zijazo kabla ya huduma hiyo kurejeshwa kikamilifu.

Mugonyi aliwaagiza watoa huduma kuchukua hatua madhubuti ili kupata njia mbadala za huduma yao na anafuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuhakikisha kuwa muunganisho wa intaneti unaoingia na kutoka unapatikana.