Wanawake kufuatilia mali za waume zao
2024-05-17 08:13:22| CRI

Wanawake wengi katika ndoa wamekuwa wakijikuta tegemezi kwa waume zao, hasa linapokuja suala la mali zinazochumwa kwenye ndoa. Ukiukwaji wa haki hizi hupelekea wanawake kubakia masikini na hukosa fursa sawa na wanaume. Hali hii huwafanya waishi maisha duni na kila mara katika hatari ya kunyanyaswa na wazazi na mashemeji. Matokeo ya vitendo hivi ni nchi kushindwa kuendelea.

Hata hivyo hapa nchini China, serikali ya mkoa wa Fujian, imeamua kuvunja mipaka hiyo na kuanzisha sheria inayowaruhusu wanawake kukagua mali za waume zao. Sheria hii vilevile inatekelezwa katika baadhi ya miji nchini China. Hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake hasa katika suala la kuepuka kukiuka haki za wanawake. Wanandoa wanapochuma mali pamoja wote wawili wana haki juu ya mali hizi, lakini kwa kuwa mara nyingi imezoelekea kuwa wanaume ndio wachumaji, wanawake huonekana hawana haki nazo, wakati huohuo ikisahaulika kwamba mwanamke naye ana mkono wake kwenye mali hizo hadi zikaweza kupatikana. Hivyo kwenye kipindi cha ukumbi wa wanawake leo tutaangalia wajibu wa wanawake kuchunguza na kujua mali anazochuma na mumewe kwenye ndoa.