China yasema kauli ya "uwezo wa uzalishaji kupita kiasi" ya Marekani inatumika kukandamiza viwanda vyenye nguvu vya nchi nyingine
2024-05-15 09:29:12| CRI

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Wang Wenbin amesema Marekani kimsingi inatumia kauli ya "uwezo wa uzalishaji kupita kiasi" kuvishinda viwanda vyenye nguvu vya nchi nyingine, kujilinda na kukanyaga kanuni za soko na sheria za biashara za kimataifa kwa jina la "ushindani wa haki".

Wang aliyasema hayo Jumanne katika mkutano na wanahabari alipokuwa akijibu kauli ya hivi karibuni ya Waziri wa Fedha wa Marekani Janet Yellen kuhusu "uwezo wa uzalishaji kupita kiasi wa China".

Wang alifafanua kuwa kwa mantiki ya Marekani, ruzuku za Marekani ni "za uwekezaji katika viwanda muhimu", wakati huohuo ruzuku za nchi nyingine zinaonekana kama "usumbufu wa ushindani usio wa haki", akiongeza kuwa mauzo ya nje ya Marekani yenye faida linganishi ni "biashara huria," huku mauzo ya nje ya nchi nyingine yenye faida linganishi ni ishara za "uwezo wa uzalishaji kupita kiasi".

Wang alisema hatua ya Marekani ni ya uonevu tu. Amesisitiza kwamba ukuaji wa kasi wa sekta mpya za nishati za China unatokana na uvumbuzi endelevu wa teknolojia, minyororo kamili ya viwanda na usambazaji na ushindani kamili wa soko, na uwezo wa China ni matokeo ya faida linganishi na sheria za soko kwa pamoja, sio kwa kile kinachojulikana kama "ruzuku".