Idadi ya vifo vya watu yafikia 33 katika jengo lililoporomoka nchini Afrika Kusini
2024-05-15 09:32:19| CRI

Kufuatia kuporomoka kwa jengo nchini Afrika Kusini, kazi za uokoaji zinaendelea kwa wiki ya pili sasa na idadi ya vifo vya watu imepanda na kufikia 33.

Miongoni mwa mafundi 81 wanaojenga jengo hilo, 62 wameokolewa au kupatikana, na wengine 19 bado hawajapatikana. Jumla ya wanaume 27 na wanawake 6 wametangazwa kufariki baada ya jengo hilo kuporomoka. Mamlaka zinakabiliwa na changamoto katika kuwatambua wahanga hao hivyo wameomba msaada kwa wananchi kwani kati yao ni sita pekee ndio wametambuliwa hadi sasa.

Serikali ya manispaa ya George imetoa taarifa na kusema kwamba wanakumbana na ugumu wa kupata majina sahihi ya watu walionasa kwenye vifusi au kufariki, hivyo wameziomba familia ambazo zimepoteza mawasiliano na wapendwa wao kufika haraka katika Kituo cha George Civic kwenye Mtaa wa York. Na kusisitiza kwamba hatua hiyo itaiwezesha Idara ya Maendeleo ya Jamii kukusanya taarifa za kina na za uhakika, ili kuhakikisha rikodi zote zinaandikwa kwa usahihi.