Wataalamu wakutana nchini Kenya ili kukuza ufikiaji wa kidijitali barani Afrika
2024-05-15 09:26:39| CRI

Wataalamu wameanza mkutano wa siku tatu mjini Nairobi, Kenya, ili kuhimiza upatikanaji wa kidijitali na teknolojia saidizi kwa watu wanaoishi na ulemavu katika bara zima la Afrika.

Mkutano huo wa 5 wa Umoja wa Afrika wa 2024 unaofanyika chini ya kaulimbiu "Kuvunja Vikwazo: Kuboresha Upatikanaji wa Kidijitali kwa Mustakabali Jumuishi wa Watu wenye Ulemavu Barani Afrika", uliwaleta pamoja zaidi ya washiriki 300, wakiwemo wataalamu, wavumbuzi, wajasiriamali na maafisa wa serikali kutoka kote barani Afrika ili kubadilishana maarifa juu ya namna ya kuondokana na vikwazo vilivyopo vya ujumuishaji wa kidijitali.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, mjumbe maalum wa Kenya katika masuala ya teknolojia, Phillip Thigo, alisema wakati zama hizi zinashuhudia maendeleo makubwa zaidi ya kiteknolojia, Afrika pia inashuhudia kuongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa teknolojia, hasa miongoni mwa watu wanaoishi na ulemavu barani Afrika. Ameongeza kuwa teknolojia zinazoibukia kama vile blockchain zinaweza kuwajumuisha kifedha watu wenye ulemavu kwa kupanua ufikiaji wa huduma za benki na mikopo ambazo zinaweza kuwa hazipatikani hapo awali.