Mazungumzo ya upatanishi nchini Kenya yanalenga kuimarisha mchakato wa uchaguzi nchini Sudan Kusini
2024-05-15 09:33:53| CRI

Mazungumzo ya ngazi ya juu ya upatanishi wa Sudan Kusini, yanayoendelea mjini Nairobi, Kenya, yataongeza msukumo katika mchakato wa uchaguzi ujao nchini humo.

Hayo yamesemwa na mkuu wa kitivo cha masomo ya kijamii na kiuchumi katika Chuo Kikuu cha Juba Abraham Kuol Nyuon, akiongeza kuwa mazungumzo yaliyofunguliwa Mei 3 na Rais William Ruto wa Kenya sio tu yatahamasisha nchi nzima ya Sudan Kusini kwa uchaguzi mkuu ujao bali pia yataweka msingi wa amani ya kudumu nchini humo kwa kushirikisha makundi yote ya upinzani yaliyosalia.

Kuol ameliambia shirika la habari la China Xinhua kuwa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa imeona uwezekano wa kuleta kila mtu kwenye bodi kabla ya kuweza kuzungumza juu ya uchaguzi.

Sudan Kusini inatazamiwa kufanya uchaguzi mwezi Desemba, kwani kipindi cha mpito kilichoongezwa Agosti 2022 kitakamilika Februari 2025. Kuol alisema makubaliano ya amani ya Nairobi yataunganishwa na Makubaliano Yaliyofikiwa tena Mwaka 2018 kuhusu Utatuzi wa Mizozo nchini Sudan Kusini, ambayo yalisuluhishwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya nchi za Afrika Mashariki (IGAD) kumaliza mgogoro wa miaka mingi tangu Desemba 2013.

Habari nyingine zinasema kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), zaidi ya watu milioni 7 kati ya watu wanaokadiriwa milioni 11 wa Sudan Kusini huenda wakakumbwa na kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula hadi Julai. OCHA imesema ghasia kati ya jamii, mgogoro wa kiuchumi na majanga yanayosababishwa na hali ya hewa yanatishia angalau watu 79,000 wanaokabiliwa na hatari kubwa ya janga la njaa.