Tanzania kufunga kamera 6,500 ili kuimarisha usalama katika miji mikubwa minne
2024-05-16 09:11:34| CRI

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tanzania Jumatano ilisema itafunga kamera 6,500 kwenye maeneo makuu ya kiuchumi ya miji minne mikubwa ili kuimarisha usalama.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Hamad Masauni alisema ufungaji wa kamera hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa “miji salama”, ambao utaanza katika mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Masauni alitangaza mipango hiyo alipowasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 bungeni Dodoma. Alisema kamera hizo zenye teknolojia ya kisasa ya akili bandia zitafungwa kwenye maeneo ya viwanda, maeneo ya kibiashara, sehemu za mikusanyiko, barabara za miji, hoteli na sehemu za huduma za jamii katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.