Kiongozi wa Kenya atafuta msaada wa kijeshi ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa
2024-05-16 09:13:38| CRI

Rais wa Kenya William Ruto Jumatano alitoa wito kwa jeshi la nchi hiyo kuisaidia serikali kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza wakati wa gwaride la kumaliza mafunzo kwa maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika Chuo cha Mafunzo ya Makuruta huko Eldoret, Ruto alisema mabadiliko ya tabia nchi ni tishio kubwa kwa maendeleo na ustawi wa nchi. Amefafanua kuwa wakati wanalinda taifa lao dhidi ya vitisho vya usalama vinavyoibuka, mabadiliko ya tabia nchi pia yatakuwa kitisho kikubwa, na kuongeza kuwa ndio maana lazima wahamasishe jeshi kutoa suluhisho kwa maswala yanayoibuka. Kiongozi huyo wa Kenya alisema wanajeshi wanapaswa kuongoza kwa kutoa mbinu, wakishirikiana na Wizara ya Mazingira, ili kufikia lengo la upandaji miti bilioni 15 ifikapo 2032.

Wakati huohuo Mamlaka ya Kitaifa ya Kudhibiti Ukame (NDMA) imesema mvua kubwa zimesababisha kaunti 23 katika ardhi kame na nusu kame nchini Kenya, ambazo kwa kawaida huathiriwa na ukame, kukumbwa na mafuriko makubwa. Mamlaka hiyo imebainisha kuwa mafuriko hayo makubwa yamedhoofisha usalama wa chakula katika maeneo kame.