Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imefanya maziko ya watu waliouawa katika shambulio la mabomu katika kambi za wakimbizi wa ndani (IDP) mkoani Kivu Kaskazini, mashariki mwa nchi hiyo.
Waziri wa Masuala ya Kijamii, Kibinadamu na Mshikamano wa Kitaifa wa nchi hiyo Modeste Mutinga Mutushayi amesisitiza tena utayari na dhamira ya serikali ya DRC ya kufanya kila linalowezekana kurejesha amani katika sehemu ya mashariki ya nchi hiyo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuwa, hatari ya milipuko mingine ya mabomu haiwezi kupuuzwa kwa kuwa bomu moja lililoangushwa halijalipuka, na pia kuna ongezeko la vurugu katika maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi wa ndani.
Tarehe 3 mwezi huu, mabomu matano yalianguka ndani na pembezoni mwa kambi za wakimbizi wa ndani kando ya mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma, na kusababisha vifo vya watu 35 na wengine 37 kujeruhiwa.