Serikali ya Mpito ya Umoja wa Kitaifa ya Sudan Kusini na makundi ya upinzani Alhamisi walisaini makubaliano kwa ajili ya kuimarisha juhudi za kufikia amani na utulivu wa kudumu nchini humo.
Zikisaini azimio la pendekezo la Tumaini, pande hizo mbili zimeahidi kuunga mkono jitihada za kusimamisha uhasama na kuhimiza ukuaji shirikishi nchini Sudan Kusini.
Hafla ya kusaini makubaliano iliyofanyika mjini Nairobi nchini Kenya, ilishirikisha maofisa wa ngazi ya juu wa serikali, wanadiplomasia, makundi ya upinzani, asasi za kijamii na washirika wa pande mbili. Katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Kenya Abraham Korir SingOei, amepongeza kusainiwa kwa makubaliano hayo, ambayo yatahimiza kufikiwa kwa amani, haki, ushirikishi na utawala bora nchini Sudan Kusini.