Nchi katika eneo kubwa la Pembe ya Afrika zinapaswa kuwekeza katika mifumo thabiti ya tahadhari ya mapema ili kuongeza ustahimilivu wa jamii zilizoko kwenye msukosuko wa hali ya hewa.
Hayo yamesemwa na wataalam kwenye kongamano la mtandaoni lililofanyika jana Alhamisi mjini Nairobi, Kenya. Philip Omondi, mtaalamu wa mabadiliko ya hali ya hewa katika Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo ya Kituo cha Utabiri na Usimamizi wa Hali ya Hewa (ICPAC), alisema eneo hilo linahitaji hatua zenye matarajio zinazotokana na data ili kudhibiti dharura za hali ya hewa, zikiwemo ukame, mafuriko, vimbunga na moto wa msituni.
Kongamano hilo, lililoandaliwa na ICPAC na washirika wake, lililenga kuangazia jukumu muhimu la mifumo madhubuti ya tahadhari ya mapema katika kuimarisha mwitikio wa hali ya hewa katika eneo kubwa la Pembe ya Afrika.
Naye Mratibu anayeshughulikia ustahamilivu wa hali ya hewa katika Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), Phoebe Wafubwa Shikuku, alisema kuwekeza katika tahadhari za mapema kutasaidia serikali za eneo hilo kuweka mipango ya dharura pindi janga la hali ya hewa litatokea.