Idadi ya watu waliofariki kutokana na shambulio la moto katika msikiti nchini Nigeria yafikia 11
2024-05-17 10:44:28| cri

Watu wengine watano wamekufa kufuatia shambulizi la kuchoma moto kwa makusudi msikiti mmoja katika mkoa wa Kano, nchini Nigeria, na kufanya idadi ya watu waliofariki katika shambulio hilo kufikia 11, huku watu wengine 13 waliojeruhiwa katika shambulio hilo wakiendelea kupata matibabu hospitali.

Mkuu wa Polisi mkoa wa Kano, Usaini Gumel amesema, waathirika hao walikuwa na majeraha ya kuungua na moto na walikimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu baada ya tukio hilo lililotokea jumatano asubuhi katika kijiji cha Gadan, eneo la utawala la Gezawa katika mkoa huo.

Polisi wameanza uchunguzi juu ya shambulio hilo, na matokeo ya awali yanaonyesha kuwa chanzo cha shambulio hilo ni familia kugombea urithi.