Kenya na Uganda zimesaini makubaliano mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Rais William Ruto wa Kenya amesema mojawapo ya makubaliano hayo ni kuruhusu Uganda kuagiza na kusafirisha bidhaa za mafuta yaliyosafishwa kutoka mamlaka ya wazalishaji na kupitia Kenya, ili kutatua changamoto zinazokabili sekta ya mafuta ya Uganda.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda mjini Nairobi, rais Ruto pia amesema anaangazia umuhimu wa kurefusha reli ya SGR ya Kenya kutoka Naivasha hadi Kampala, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama njia endelevu na bora ya miundombinu kwa usafirishaji wa bidhaa. Nchi zote mbili zimewaagiza mawaziri wao kukusanya rasilimali kwa ajili ya mradi huu na kuripoti maendeleo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Mbali na hayo, Kenya imeahidi kushirikiana kwa karibu na Uganda katika kushughulikia changamoto za kiusalama katika kanda hiyo, pamoja na Sudan, Sudan Kusini, Somalia na DRC.