Baraza la Mpito la Utawala la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah Al-Burhan Alhamisi lilianza mazungumzo yake na kundi la upinzani SPLM tawi la kaskazini (SPLM-N) mjini Juba nchini Sudan Kusini, kwa lengo la kufungua njia ya kupitisha misaada ya kibinadamu kufuatia mapambano yanayoendelea.
Katibu mkuu wa SPLM-N Amar Amoun Deldoum alisema wanafanya mazungumzo na mamlaka ya utawala ya Sudan, ili kuruhusu msaada wa kibinadamu uwafikie watu wanaoathirika na mapambano katika jimbo la Kordofan Kusini, Blue Nile na Kordofan Magharibi, majimbo ambayo yanadhibitiwa na kundi lake.
Waziri wa Ulinzi wa Sudan Yassin Ibrahim Yassin alisema usafirishaji wa msaada wa dharura wa kibinadamu unategemea na kusitisha mapambano kwa pande zote zenye uhasama.