UNHCR yasema zaidi ya Wasomali 140,000 hawana makazi kutokana na mapigano na ukosefu wa usalama
2024-05-21 08:34:17| CRI

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema, zaidi ya watu 140,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini Somalia katika miezi minne ya mwanzo ya mwaka huu kutokana na mapigano na ukosefu wa usalama.

Mtandao wa Kusimamia Ulinzi na Watu Wanaorejea nchini humo ulio chini ya UNHCR umerekodi watu 15,280 waliokimbia makazi yao katika mkoa wa Bay, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani kwa mwezi April, ikifuatiwa na mkoa wa Mudug, ambapo watu 12,940 walikimbia makazi yao kutokana na mapigano na ukosefu wa usalama.

Shirika hilo limesema, watu milioni 2.94 nchini Somalia wamekimbia makazi yao mwaka jana, na kuongeza kuwa, mpaka kufikia mwezi uliopita, nchi hiyo inahifadhi wakimbizi 39,025 na watu wanaotafuta hifadhi, kati yao asilimia 66 ni wanawake na watoto.