Tamasha la Nane la Vijana wa China na Afrika lenye kauli mbiu ya “Kukusanya nguvu za vijana, Kujenga mambo ya kisasa kati ya China na Afrika” limefunguliwa Jumatatu mjini Beijing.
Zaidi ya wawakilishi 60 wa vijana kutoka nchi 52 za Afrika ambazo ni wanachama wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) watatembelea Beijing na mkoa wa Zhejiang, ili kukuza urafiki kati ya pande hizo mbili.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Chen Xiaodong amesema, tamasha hilo ni shughuli muhimu chini ya mfumo wa FOCAC, na kwamba matarajio ya mambo ya urafiki kati ya China na Afrika yanategemea vijana. Pia anatumai kuwa tamasha hilo litajumuisha nguvu za vijana na kuchangia katika kuhimiza ushirikiano wa kirafiki kati ya China na Afrika.
Balozi wa Senegal nchini China Bw. Ibrahima Sylla amesema, ushirikiano kati ya Afrika na China una uhai mkubwa na pia ni mfano mzuri wa kuigwa. Anatarajia kupanua mawasiliano na ushirikiano kati ya vijana wa pande hizo mbili, na kuhimiza vijana kuwa msukumo wa maendeleo ya uhusiano kati ya pande hizo mbili katika siku za baadaye.