Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesema litaipatia Tanzania mkopo wa takriban dola milioni 150 baada ya kufikia makubaliano na serikali ya Tanzania hivi karibuni. Mkopo huo unatolewa kupita Mpango wa Ukopeshaji wa ECF, na kufanya jumla ya msaada wa kifedha wa IMF chini ya mpango wa ECF kufikia dola za Marekani milioni 604.2.
Wakati huo huo, IMF imetahadharisha kuwa uhaba wa fedha za kigeni uliopo nchini Tanzania unaweza kuendelea kuwepo kwa mwaka huu, na hivyo kusababisha hatari kwa ukuaji wa uchumi ambao umekabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uhaba mkubwa wa umeme mwishoni mwa mwaka jana na mapema mwaka huu.