Bustani ya viwanda ya China na Tanzania itasaidia kuharakisha mapinduzi ya kiviwanda nchini Tanzania
2024-05-22 08:33:34| CRI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji) nchini Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, amesema Bustani ya Viwanda ya China na Tanzania, ambayo ujenzi wake unaendelea katika Mkoa wa Pwani nchini humo, itasaidia kuharakisha mageuzi ya kiviwanda nchini humo.

Akizungumza na Shirika la habari la China Xinhua jumatatu wiki hii, Prof. Mkumbo amesema bustani hiyo itakuwa ni kubwa zaidi nchini Tanzania, na itaweza kuwa na viwanda 200, na hivyo kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Amesema mwaka huu ni miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania, na uhusiano kati ya pande hizo mbili umeendelea kuwa wa kuheshimiana kwa miongo 6 iliyopita.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa bustani hiyo Janson Huang amesema, ujenzi wa bustani hiyo ulioanza mwezi Mei mwaka 2022, unatarajiwa kukamilika mwaka 2026. Ameongeza kuwa, bustani hiyo itakuwa na kanda saba ambazo ni pamoja na viwanda vya nguo, madawa, utengenezaji wa vifaa, na vifaa vya ujenzi.