Maofisa wa China na Afrika watoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili chini ya jukwaa la FOCAC
2024-05-22 08:32:26| CRI

Maofisa wa China na Ethiopia wametoa wito wa kuboresha ushirikiano wa pande nyingi kati ya China na Afrika chini ya mfumo wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).

Wito huo umetolewa katika mkutano wa ngazi ya juu wa “Kutathmini Nafasi ya Ethiopia katika FOCAC na Hatua Inayofuata” uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, hapo jana.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mkuu wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia Eshete Tilahun amesema FOCAC imedhihirisha kuwa ni jukwaa lenye nguvu na ufanisi katika kuboresha ushirikiano kati ya Afrika na China kwa kuunga mkono maendeleo ya miundombinu ya kimsingi, kuboresha muunganiko, kuinua shughuli za kibiashara, kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, na kusaidia ujasiriamali barani Afrika.

Naye Waziri Mshauri wa masuala ya uchumi katika Ubalozi wa China nchini Ethiopia Yang Yihang amesema, kutokana na mfumo wa FOCAC kutumika kama kichocheo kikubwa, ushirikiano wa China na Afrika umepata mafanikio makubwa, na kuzifanya pande hizo mbili kuwa wenzi wakubwa wa kibiashara kwa miaka 15 mfululizo.