Watu 11 wafariki baada ya mtambo wa kiwanda cha sukari nchini Tanzania kulipuka
2024-05-24 08:32:16| CRI

Watu 11 wamefariki wakiwemo raia watatu kutoka Brazil, Kenya na India na mafundi mitambo wanane Watanzania na wengine wawili kujeruhiwa vibaya mapema jana baada ya mtambo katika kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichopo mkoa wa Morogoro nchini Tanzania kulipuka.

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani humo Shaban Marujugo ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua kwa njia ya simu kuwa, mlipuko huo ulitokea majira ya saa saba usiku kwa saa za huko katika kiwanda hicho kilichoko Wilaya ya Kilombero.

Fundi umeme katika kiwanda hicho aliyefahamika kwa jina la Juma Ramadhani Palamba amesema, mlipuko huo ulitokea katika chumba cha usimamizi ambako mafundi walikuwa wakifanya majaribio ya mfumo wa mpira wa joto unaotumika katika utengenezaji wa sukari.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima ameagiza kiwanda hicho kifungwe kwa siku tatu baada ya mlipuko huo, hatua ambayo itasaidia Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kufanya uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.