Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kununua tani 500,000 mahindi Tanzania
2024-05-24 10:16:59| cri

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula wa Tanzania (NFRA), amesaini mkataba wa mauziano ya mahindi tani 500,000 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa chakula kwa nchi hiyo. Mkataba huo wameingia na kampuni moja ya Jimbo la Katanga, lengo likiwa ni kuwasaidia upatikanaji wa chakula.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweri, amesema katika awamu ya kwanza ya mkataba, DRC wataondoka na tani 200,000 na awamu nyingine watamalizia tani 300,000.

Bw. Mweri amesema wameanza ushirikiano huo wa kufanya biashara ya mazao, kama moja ya mikakati waliyoweka kwa ajili ya kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Pia amesema serikali imetenga Sh. bilioni 300 kwa ajili ya uwekezaji wa kununua mazao ya chakula tani 300,000, msimu unapoanza NFRA itaanza ukusanyaji wa mazao ya chakula.