Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito kwa nafasi ya Afrika katika mpango wa amani na usalama duniani
2024-05-24 08:33:19| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuna haja ya kuhusisha ushiriki na uongozi wa Afrika katika mpango wa amani na usalama wa duniani.

Akizungumza katika mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kuimarisha nafasi ya Afrika katika kukabiliana na changamoto za amani na usalama duniani uliofanyika jana, Guterres amesema baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mfumo wa usimamizi wa dunia, ikiwemo Baraza hilo, uliundwa na nchi zenye nguvu zaidi wakati huo, ambao nchi nyingi za Afrika zilikuwa bado zinajiondoa katika vifungo vya ukoloni.

Ameongeza kuwa, pamoja na kwamba tangu wakati huo dunia imebadilika, lakini taasisi za kimataifa bado hazijabadilika, na mpaka sasa nchi za Afrika zinaendelea kunyimwa kiti katika meza ya majadiliano, ikiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Amesema Afrika inastahili kuwa na sauti katika mpango wa amani na usalama wa dunia, lakini kuimarisha sauti ya Afrika kutawezekana pale tu nchi za Afrika zitakaposhiriki katika mifumo ya usimamizi wa dunia kwa usawa.