Mfanyakazi wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka auawa katika mapigano nchini Sudan
2024-05-27 14:14:10| cri

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema mmoja wa wafanyakazi wake ameuawa katika mji mkuu wa mkoa wa Darfur Kaskazini, El Fasher, nchini Sudan.

Mfanyakazi huyo aliuawa jumamosi baada ya kombora kuanguka katika nyumba yake iliyo karibu na soko kuu la mjini hapo, na alifariki hospitali wakati akipatiwa matibabu.

Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ya Sudan, MSF imetibu zaidi ya wagonjwa 930 katika Hospitali ya El Fasher Kusini tangu mapigano yalipoanza kati ya Jeshi la Sudan na Kikosi cha Mwitikio wa Haraka (RSF) katika mji huo wiki mbili zilizopita.