Tanzania na Uganda zaungana kuendeleza azma ya ushirikiano katika ukuzaji wa viwanda
2024-05-27 08:44:28| CRI

Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania ambaye pia ni Waziri wa Nishati Doto Biteko amesema serikali za Tanzania na Uganda zimekubaliana kushirikiana katika kutekeleza azma ya nchi hizo mbili za ukuzaji wa viwanda. Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa ufungaji wa kongamano la pili la biashara kati ya Tanzania na Uganda Ijumaa jioni. 

Kongamano hilo lililokuwa na lengo la kutafuta njia za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, lilifanyika jijini Dar es Salaam. Biteko alisema nchi hizo mbili zimeazimia kusukuma mbele ajenda ya ukuzaji wa viwanda kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ikiwemo barabara, reli na umeme ili kusaidia utekelezaji wake kwa ufanisi.

Amebainisha kuwa nchi zote mbili zimejikita katika kuendeleza viwanda vya usindikaji vitakavyosaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na madini na kuongeza kuwa Tanzania na Uganda zilisaini makubaliano katika sekta ya nishati. Biteko aliongeza kuwa kongamano hilo pia liliazimia kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.