Tume ya Uchaguzi nchini Afrika Kusini yalaani vitisho dhidi ya wafanyakazi wake
2024-05-27 14:15:05| cri

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Afrika Kusini (IEC) imelaani vitisho vilivyotolewa dhidi ya maofisa na wafanyakazi wake katika mkoa wa KwaZulu-Natal.

Ofisa mkuu wa Tume hiyo, Sy Mamabolo amesema, hakuna chama wala wawakilishi wake wenye mamlaka ya kwenda katika makazi binafsi ya wafanyakazi wa tume hiyo, na kuongeza kuwa, hakuna chama wala wawakilishi wake wanaweza kudhibiti vifaa vya uchaguzi bila ya kupewa kibali cha kufanya hivyo.

Amesema ofisa mmoja wa Tume hiyo alivamiwa nyumbani kwake jumamosi usiku na watu waliotaka kujua kuhusu vituo vya kupigia kura, mabango ya vituo vya kupigia kura, na maboksi mapya ya kuhifadhia kura, vitu vilivyohifadhiwa katika kituo cha kupiga kura kilichopo Chesterville mkoani humo.