Madhara ya kuvuta sigara kwa wanawake na watoto
2024-05-31 08:16:04| CRI

Watu wengi wanajua kuwa uvutaji wa sigara na tumbaku huleta hatari na madhara mengi mwilini. Lakini cha kustaajabisha ni kwamba bado wanaendelea kuvuta bila kujali madhara yake. Madhara hayo ni pamoja na saratani ya mapafu na matatizo ya kupumua, na watu wachache tu wanatambua kwamba pia huongeza sana hatari ya ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa mishipa ya pembeni (ugonjwa katika viungo vinavyosambaza damu kwenye mikono na miguu) na kupanuka kwa mishipa ya aota.

Jambo ambalo watu wengi hawafahamu ni kwamba uvutaji wa shisha una madhara mengi kuliko uvutaji wa sigara. Hii ni kwasababu ya muda na idadi ya moshi unaovutwa. Mtu anayevuta sigara huwa anavuta mililita 30 ya moshi mara ishirini. Lakini mtu anayevuta shisha kwa saa moja, huwa anavuta mililita 500 ya moshi mara 200. Kwa ujumla anayevuta sigara anavuta takriban mililita 600 ya moshi wakati anayevuta shisha anavuta mililita 100,000 ya moshi kwa ujumla. Hivyo, mvutaji wa shisha huvuta moshi wa idadi ya sigara 100. Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (THDS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaeleza kuwa kiwango cha wanawake wanaovuta sigara ni asilimia moja. Hivyo leo katika ukumbi wa wanawake tutaangalia madhara ya uvutaji wa sigara na shisha kwa wanawake.