Marais wa China na Guinea ya Ikweta wafanya mazungumzo Beijing
2024-05-29 08:56:33| CRI

China na Guinea ya Ikweta jana Jumanne zilitangaza kuinua uhusiano wao hadi kufikia ngazi ya Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati wa Pande Zote.

Uamuzi huo ulitangazwa na Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wakati walipofanya mazungumzo hapa Beijing.

Rais Xi amesema, China na Guinea ya Ikweta ni marafiki wakubwa na wenzi wazuri, na uhusiano kati yao unaakisi kiwango cha juu cha kuaminiana kisiasa. China inaiunga mkono kithabiti Guinea ya Ikweta kulinda mamlaka na uhuru wa taifa, kupinga uingiliaji wa nje na kutafuta njia ya kujiendeleza inayofaa hali yake halisi.

Naye Rais Obiang amesema, tangu China na Guinea ya Ikweta zianzishe uhusiano wa kibalozi miaka 54 iliyopita, uhusiano wao umekuwa ukidumisha maendeleo ya kirafiki na sasa uko kwenye kipindi kizuri zaidi katika historia. Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili siku zote umekuwa ukifanyika kwa msingi wa usawa na kuheshimiana, na wala sio kwa kulazimishana.