Kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei Jumanne ilitoa zawadi mbalimbali, yakiwemo makombe, vyeti na vifaa vya kielektroniki, kwa washindi wa hackathon wenye mahitaji maalum, ambayo ilizinduliwa nchini Kenya mwezi Machi.
Washindi hao wakiwemo wanafunzi wa chuo cha Huawei ICT, walitambuliwa kwa kutoa suluhisho bora ya kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu. Maafisa wakuu wa serikali na watendaji wa Huawei walihudhuria hafla hiyo ya utoaji tuzo, iliyofanyika kando ya mikutano ya kila mwaka ya Benki ya Maendeleo ya Afrika jijini Nairobi.
Mtaalamu wa mahusiano ya umma katika kampuni ya Huawei Kenya, Winnie Chepkonga, alisema mashindano ya hackathon ya Akili Bandia (AI) ni muhimu kwa ajili ya kuhimiza wanafunzi kuvumbua kwa manufaa ya wale walio na ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Maalum ya Kenya, Norman Kiogora, alisema kupitia ushirikiano na Huawei, taasisi hiyo itaweza kuimarisha upatikanaji wa teknolojia zinazowawezesha watu wanaoishi na ulemavu. Kiogora alisisitiza kuwa kwa kutumia AI, watu wenye mahitaji maalum wanaweza kupata ujuzi wa maisha, kuunganishwa katika uchumi wa kawaida, na kuwa na ufahamu zaidi wa mazingira yao.