Rais wa China akutana na mwenzake wa Misri
2024-05-29 19:22:29| cri

Rais Xi Jinping wa China leo tarehe 29 hapa Beijing alifanya mazungumzo na Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri, ambaye alikuja China kushiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Nchi za Kiarabu na kufanya ziara ya kitaifa.

Akimpongeza Abdel Fattah el-Sisi kwa kuchaguliwa tena kuwa rais wa Misri, Rais Xi Jinping amesema mwaka huu unaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa ushirikiano wa kimkakati kwa pande zote kati ya China na Misri. Katika miaka 10 iliyopita, chini ya uongozi wa marais wa nchi hizo mbili, uhusiano wa China na Misri umekuwa mfano hai wa ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na nchi za Kiarabu, Afrika, nchi za kiislamu na nchi zinazoendelea.

Ameongeza kuwa dunia ya leo inakabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea kwa karne moja, ambayo mengi ni matatizo na changamoto kubwa. China inatetea kujenga dunia yenye ncha nyingi na utandawazi jumuishi, na kupenda kuimarisha hali ya kuaminiana kati yake na Misri, kuendeleza ushirikiano, na kulinda kwa pamoja haki na usawa wa kimataifa pamoja na maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, na kuchangia amani, utulivu, maendeleo, na ustawi wa kanda na dunia nzima.